Serikali ya kaunti ya Kilifi imezindua kituo cha matibabu ya dharura ya figo ambacho kina vifaa vyote hitajika, wahudumu na ambulensi za kisasa zilizo na vifaa hitajika kushughulikia visa vya dharura kwenye kaunti hiyo.
Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro alizindua kituo hicho pamoja na ghala la kuweka dawa zitakazokuwa zikisambazwa kwenye vituo vingine vya afya.
Alisema kituo hicho kwa sasa kina vitanda vitatu lakini katika muda wa wiki mbili zijazo kitaongezewa vitanda vingine 13 na kuwa na vitanda 16 kwa jumla.
“Sasa wagonjwa wa matatizo ya figo waliokuwa wakisafiri mwendo mrefu kupata huduma za afya wanaweza kutibiwa katika hospitali ya Kilifi badala ya kwenda Mombasa au Malindi” alisema Mung’aro.
Gavana huyo alisema wamesajili watu 8000 kwenye bima ya kitaifa ya matibabu NHIF na wametenga shilingi milioni 60 ili kusajili wakazi zaidi wa kaunti ya Kilifi kwa bima hiyo.
Huduma za ambulensi alisema ni za bure bila malipo ndani ya kaunti ya Kilifi na mgonjwa atagharamika tu iwapo anataka ambulensi impeleke kwenye hospitali isiyo ya serikali kwani atakuwa ameonyesha ana pesa za kutosha kupata huduma kwenye kituo kama hicho.
Naibu gavana Kilifi Flora Chibule alisema hatua ambazo serikali ya kaunti inapiga kwenye sekta ya afya zitapunguza malalamishi kuhusu huduma za afya. Alitaja miradi inayotekelezwa kuwa baraka.
Waziri wa afya katika serikali ya kaunti ya Kilifi Peter Mwarogo alisema kituo kilichozinduliwa cha matibabu ya figo, kitapunguza msongamano katika hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi.
Ghala lililozinduliwa alisema linalenga kuhakikisha uwepo wa dawa za kutosha kusambaza kwa hospitali zote za kaunti ya Kilifi.