Kituo cha masomo ya kupambana na ufisadi Afrika chazinduliwa Nairobi

Kituo hicho ni cha kwanza na cha aina yake kuwahi kuzinduliwa barani Afrika.

Martin Mwanje
3 Min Read
Wajumbe wakihudhuria kongamano la AAACA jijini Nairobi

Kituo cha Masomo na Utafiti wa Kupambana na Ufisadi barani Afrika kimezinduliwa leo Jumanne jijini Nairobi. 

Kituo hicho ni cha kwanza na cha aina yake kuwahi kuzinduliwa barani Afrika.

Kilizinduliwa rasmi na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor kwa niaba ya Rais William Ruto pamoja na Rais wa Umoja wa Mamlaka za Kupambana na Ufisadi barani Afrika (AAACA) Jenerali Hisham El Rakaybi walioandamana na wajumbe wengine wanaohudhuria kongamano la siku tatu la AAACA linalofanyika jijini Nairobi.

Kituo hicho kitatumiwa kwa utafiti, uvumbuzi, uendelezaji wa sera, ukuzaji wa uwezo na mabadilishano ya maarifa miongoni mwa nchi za Afrika katika jitihada zao za pamoja za kutokomeza ufisadi barani humo.

Pia kitasaidia kutambua hatari ibuka, kutathmini hatua zinazofaa kuchukuliwa na mageuzi yanayopaswa kufanywa ili kuimarisha asasi za kukabiliana na ufisadi na matokeo ya uongozi.

Oduor, aliyemwakilisha Rais Ruto kwenye kongamano hilo, alilalamikia mabilioni ya pesa zinazopotea kupitia kwa ufisadi barani Afrika badala ya kutumiwa kuliendeleza bara hilo.

“Naipongeza AAACA kwa uongozi wake endelevu na dhamira isiyoyumba ya kuimarisha mifumo yetu ya uadilifu barani Afrika. Pia nawapongeza wadau wote ambao kujitolea kwao na maoni yamechangia kuanzishwa kwa Kituo Kituo cha Masomo na Utafiti wa Kupambana na Ufisadi barani Afrika,” alisema Oduor wakati akihutubia hadhira kwenye kongamano hilo.

“Mikakati iliyofanikiwa zaidi ya kupambana na ufisadi ni ile inayochanganya uzuiaji, utekelezaji, elimu ya umma, urejeshaji wa mali, uwazi, na ushiriki wa wananchi katika mpangokazi wa pande mbili unaoeleweka na kutekelezwa.”

Awali, mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini Kenya, EACC Dkt. David Oginde alielezea umuhimu wa mamlaka za kupambana na ufisadi barani Afrika.

“Naamini kuwa sisi ndio tumaini la Afrika katika kupambana na ufisadi. Maudhui ya kuimarisha ushirikiano na ubunifu kwa ajili za jitihada zifaazo za kupambana na ufisadi ni azimio letu la pamoja kwamba hakuna asasi hata moja inaweza kukabiliana na tatizo hili peke yake; tunahitaji kufanya kazi pamoja,” alisema Dkt. Oginde.

“Tunahitaji kuimarisha uwezo wa asasi zetu kwa kukumbatia ubunifu. Mfumo wa dijitali unakuwa mgumu zaidi kufanya kazi nao, kwa kutumia mifumo ya awali. Lazima tuwe wabunifu na kutumia akili unde, AI, block chain na teknolojia zingine za kisasa zinazoweza kutumiwa kudhibiti uhamishaji wa rasilimali haraka zaidi.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa EACC Abdi Mohamud alielezea matarajio walio nayo  wananchi kwa mamlaka za kupambana ufisadi kusaidia kuangamiza zimwi hilo.

“Wananchi wanatarajia mamlaka za kupambana na ufisadi kuonyesha matokeo dhahiri kupitia ufuatiliaji, kushikilia, kunasa na kurejesha mali zilizopatikana kupitia uhalifu na ufisadi,” alisema Mohamud wakati wa ufunguzi rasmi wa kongamabo hilo la siku tatu lililoanza hapo jana.

Kongamano Kuu la 8 la kila mwaka la Mamlaka za Kupambana na Ufisadi (AAACA) linawaleta wajumbe zaidi ya 150 kutoka barani Afrika na limepangiwa kumalizika kesho Alhamisi.

Share This Article