Kisa kipya cha Mpox chanakiliwa hapa nchini

Tom Mathinji
2 Min Read

Taifa hili limenakili kisa kipya cha ugonjwa wa Mpox katika muda wa saa 24 zilizopita na kufikisha idadi jumla ya visa vya ugonjwa huo vilivyonakiliwa hapa nchini kuwa 10.

Kulingana na taarifa kutoka wizara ya afya leo Alhamisi, mwathiriwa wa kisa hicho ni mwananmke mwenye umri wa miaka 35 kutoka kaunti ya Kericho.

Visa hivyo vinajumuisha 2 vilivyoripotiwa katika kaunti ya Nakuru huku kaunti za Taita Taveta, Busia, Nairobi, Mombasa,, Makueni,, Kajiado,Bungoma na Kericho zikinakili kisa kimoja kila kaunti.

Katika taarifa hiyo iliyotiwa saini na waziri wa afya Dkt. Deborah Barasa, ilithibitisha kuwa hakuna kifo ambacho kimenakiliwa hapa nchini kutokana na ugonjwa huo hadi kufika sasa.

“Juhudi zetu za uangalizi zinasalia imara na Wizara imewafuatilia watu 68 wanaoshukiwa kuambukizwa ugonjwa huo. 61 kati yao wamefuatiliwa kwa kipindi kilichopendekezwa cha siku 21, na waliosalia saba wanafuatiliwa na timu zetu za afya ya umma katika kaunti husika na wahudumu wa afya ya jamii,” alisema Barasa.

Kulingana na Waziri Barasa, ni mtu mmoja tu kati ya watu hao aliyebainika kuambukizwa ugonjwa wa Mpox katika kipindi hicho cha ufuatiliaji.

Ameongeza kuwa wizara yake inaendelea kuwapima wasafiri katika maeneo yote ya kuingia nchini.

Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, wasafiri 15,541 wamepimwa ugonjwa huo na kufanya idadi ya jumla ya wasafiri waliopimwa katika maeneo 26 ya kuingia nchini kufikia 1,128,976.

Wizara ya Afya inatoa wito kwa Wakenya kuchukua hatua za kuepuka kuambukizwa ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuepuka kutangamana na watu walioambukizwa au wanaoonyesha dalili za kuambukizwa ugonjwa wa Mpox na kuepuka kugusa vitu vilivyotumiwa na watu walioambukizwa ugonjwa huo kama vile malazi.

Share This Article