Kisa kimoja zaidi cha ugonjwa wa Mpox kimethibitishwa nchini katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Hii inafanya jumla ya idadi ya visa vilivyoripotiwa nchini kufikia 9 hadi kufikia sasa.
Visa hivyo vinajumuisha 2 vilivyoripotiwa katika kaunti ya Nakuru, Taita Taveta (1), Busia (1), Nairobi (1), Mombasa (1), Makueni (1), Kajiado (1) na Bungoma (1).
Wizara ya Afya inasema kisa cha hivi punde kilihusisha mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 37 anayefanya kazi kama dereva wa lori na alikuwa amesafiri katika nchi za Uganda na Rwanda.
“Kisa hicho kilitambuliwa na timu yetu ya uangalizi katika kaunti ya Nakuru,” amesema Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa katika taarifa.
“Juhudi zetu za uangalizi zinasalia imara na Wizara imewafuatilia watu 68 wanaoshukiwa kuambukizwa ugonjwa huo. 61 kati yao wamefuatiliwa kwa kipindi kilichopendekezwa cha siku 21, na waliosalia saba wanafuatiliwa na timu zetu za afya ya umma katika kaunti husika na wahudumu wa afya ya jamii.”
Kulingana na Waziri Barasa, ni mtu mmoja tu kati ya watu hao aliyebainika kuambukizwa ugonjwa wa Mpox katika kipindi hicho cha ufuatiliaji.
Ameongeza kuwa wizara yake inaendelea kuwapima wasafiri katika maeneo yote ya kuingia nchini.
Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, wasafiri 15,541 wamepimwa ugonjwa huo na kufanya idadi ya jumla ya wasafiri waliopimwa katika maeneo 26 ya kuingia nchini kufikia 1,128,976.
Wizara ya Afya inatoa wito kwa Wakenya kuchukua hatua za kuepuka kuambukizwa ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuepuka kutangamana na watu walioambukizwa au wanaoonyesha dalili za kuambukizwa ugonjwa wa Mpox na kuepuka kugusa vitu vilivyotumiwa na watu walioambukizwa ugonjwa huo kama vile malazi.