Kipyegon na Moraa kuwania donge nono mbio za Athlos nchini Marekani

Dismas Otuke
2 Min Read
Faith Kipyegon

Bingwa mara tatu wa Olimpiki Faith Kipyegon na bingwa wa dunia katika mita 800 Mary Moraa na Susan Ejore ni Wakenya pekee watakaoshiriki makala ya kwanza ya mbio za Athlos zitakazoandaliwa kesho, Septemba 26 mjini New York nchini Marekani.

Shindano hilo ambalo ni la wanawake pekee litakuwa la mwisho kwa Kipyegon na Moraa mwaka huu katika mbio za uwanjani.

Kipyegon na Moraa wanassiriki mashindano hayo wakiwa roho juu baada ya kutwaa ubingwa wa Diamond League katika mkondo wa mwisho wa Brussels, Ubelgiji.

Kwa upande wake, Ejore ambaye ni Mkenya anayeishi nchini Marekani pia anajivunia kushiriki michezo ya Olimpiki mwezi jana nchini Ufaransa kwa mara ya kwanza.

Kipyegon ambaye ni mshikilizi wa rekodi za Dunia katika mita 1,500 na maili 1 atatashiriki mita 1,500 akishindana na mshikilizi wa rekodi ya Dunia katika mita 5,000 Gudaf Tsegay wa Ethiopia na mshindi wa nishani ya fedha ya dunia katika mita 1,500 Deribe Welteji kutoka Ethiopia.

Wapinzani wengine ni Katie Snowden wa Uingereza, Cory MCgee wa Marekani na Susan Ejore wa Kenya.

Moraa atatimka mita 800 pamoja na Natoya Goule Toppin wa Jamaica, bingwa wa zamani wa dunia Halimah Nakaayi wa Uganda, Nia Akins wa Marekani, Addy Weiley wa Marekani na bingwa wa Dunia wa mashindano ya ukumbini Tsige Duguma kutoka Ethiopia.

Mbio hizo pia zitawashirikisha mabingwa wa Olimpiki Gabby Thomas na Marielaidy Paulinho wa Jamhuri ya Dominika watakaoshiriki mita 200 na 400 mtawalia.

Mashindano hayo yanaandaliwa na Alexis Kerry Ohanian, mumewe bingwa mara 23 wa mashindano ya Grand Slam katika mchezo wa tenisi Serena Williams wa Marekani.

Mshindi wa kila fani atatuzwa shilingi milioni 7.6 za Kenya ambayo ni maradufu ya zawadi ya pesa wanazotuzwa washindi wa Diamond League.

Website |  + posts
Share This Article