Kipyegon ateuliwa kuwania tuzo ya mwanariadha bora wa mwaka

Dismas Otuke
2 Min Read
Faith Kipyegon

Bingwa mara mbili wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 Faith Kipyegon ameteuliwa kuwania tuzo ya mwanariadha bora wa mwaka huu kwa wanawake.

Kipyegon ambye pia ni bingwa mara mbili wa dunia alifikia makuu mwaka huu, akivunja rekodi tatu za dunia katika kipindi cha mwezi mmoja katika mbio za mita 1,500, maili moja na mita 5,000.

Mwanariadha huyo aliye na umri wa miaka 29, pia alishinda dhahabu mbili za dunia katika mashindano ya Budapest mwezi Agosti katika mita 1,500 na mita 5,000.

Kipyegon anawania tuzo hiyo pamoja na bingwa wa Berlin marathon Tigist Asefa wa Ethiopia, mabingwa wa dunia Femke Bol wa Uholanzi, Shericka Jackson wa Jamaica, Haruka Kitaguchi wa Japani,Yaroslava Mahuchikh kutoka Ukraine, Maria Perez wa Uhispania, Gudaf Tsegay wa Ethiopia, Sha’Carri Richardson wa Uingereza, Yulimar Rojas kutoka Venezuela na Winfed Yavi wa Bahrain.

Mshindi atabainika kupitia kwa kura zitakazopigwa na mashabiki mitandaoni ambapo unahitaji kuweka “like” kwa mwanariadha unayempigia kura katika mitandao ya Facebook, X, Instagram na YouTube na upigaji kura utafungwa Oktoba 28, kabla ya Baraza Kuu la Shirikisho la Riadha Duniani kupiga kura ambayo itakuwa asilimia 50.

Orodha hiyo itapunguzwa hadi wanariadha watano kati ya  Novemba 13 na 14 na mshindi kubainika Disemba 11.

Share This Article