Kindumbwendumbwe cha AFCON kitaingia awamu ya 16 bora siku ya Jumamosi Januari 27 kwa mechi mbili.
Palancas Negras kutoka Angola watafungua ratiba dhidi ya Brave Warriors ya Namibia, kuanzia saa mbili usiku ikiwa derby ya COSAFA.
Timu zote zinacheza raundi ya 16 bora kwa mara ya kwanza huku Angola, ikijivunia kutoshindwa na Namibia.
Angola iliongoza kundi D, wakishinda mechi mbili na kutoka sare huku Namibia, ikimaliza ya tatu kundini E.
Baadaye saa tano usiku Cameroon itakumbana na Nigeria katika mechi ya pili ikiwa derby ya Afrika magharibi.
Nigeria ukipenda Super Eagles walimaliza wa pili kundini A,huku Cameroon wakichukua nafasi ya pili kundini B.
Jumapili itakuwa zamu ya Equatorial Guinea kukabana koo na Guinea, kabla ya Misri kumaliza udhia ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo.
Jumatatu Cape Verde watapimana nguvu na Mauritania timu zikicheza raundi ya 16 kwa mara ya kwanza, kisha baadaye saa tano usiku wenyeji Ivory Coast wakabiliane na mabingwa watetezi Senegal.
Jumanne Mali watapambana na Burkina Faso, katika derby ya Afrika magharibi, huku Morocco wakihitimisha ratiba dhidi Afrika Kusini.