Amos Kipruto na bingwa mara mbili Ruth Chepng’etich watashiriki makala ya 46 ya mbio za Chicago Marathon kesho Oktoba 13 nchini Marekani .
Mbio za wanaume kesho zitakuwa na hisia kali kwani ni katika makala ya mwaka jana ambapo marehemu Kelvin Kiptum alishinda na kuweka rekodi mpya ya dunia ya saa 2 na sekunde 35,kabla ya kufariki miezi minne baadaye kupitia ajali ya barabarani.
Kipruto anayejivunia muda bora wa saa 2 dakika 3 na sekunde 13 anapigiwa upato kutwaa ubingwa katika mbio za wanaume baada ya kutatizwa na msururu wa majeraha .
Wakenya wengine watakaoshiriki ni Vincent Kipkemoi Ngetich,Daniel Ebenyo na John Korir wakimenyana na Birhanu Legese wa Ethiopia aliye na muda wa kasi zaidi wa saa 2:02:48 alioandikisha mwaka 2019 katika mbio za Berlin Marathon.
Katika mbio za wanawake Chepng’etich atarejea kulipiza kisasi baada ya kumaliza wa pili mwaka uliopita kwa saa 2 dakika 15 na sekunde 37, na atashindana na Wakenya mwenza Joyciline Jepkosgei,Irine Cheptai,Dorcas Tuitoek, Mary Ngugi na Stacey Ndiwa.