Katibu katika Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Dkt. Kipronoh Ronoh leo Jumatano amezindua awamu ya nane ya maonyesho ya bara Afrika ya kilimo na mustakabali wa chakula na mifugo jijini Nairobi nchini Kenya.
Maonyesho hayo ya siku mbili ambayo ni pamoja na kongamano, yanaandaliwa katika jumba la mikutano ya kimataifa la Kenyatta KICC.
Mada ya mkutano huo ni “Kubadili mifumo ya kilimo na chakula na biashara inayonoga barani Afrika: Uvumbuzi, uendelevu na uwekezaji kwa mustakabali stahimilivu”.
Umawaleta pamoja waunda sera, viongozi wa tasnia, wajasiriamali wa kilimo, wakulima, watafiti na watoaji huduma za kiteknolojia toka kote ulimwenguni.
Maonyesho hayo ni jukwaa kwa wanaohudhuria kongamano hilo kubadilishana mawazo, ujuzi, kufahamiana na kuonyesha teknolojia za kipekee pamoja na uvumbuzi unaolenga kuimarisha usalama wa chakula nchini Kenya na barani Afrika.