Kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye akamatwa

Tom Mathinji
1 Min Read
kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye.

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye, anadaiwa kutekwa nyara na kuzuiliwa katika kambi moja ya kijeshi Jijini Kampala Uganda.

Haya yalifichuliwa na mke wake Winnie Byanyima ambaye ni afisa mkuu katika shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada la UNAIDS.

Kupitia mtandao wake wa X, Winnie alisema Besigye alikamatwa akiwa Jijini Nairobi baada ya kuhudhuria hafla ya kuzinduliwa kwa kitabu cha mwanasiasa Martha Karua.

“Alitekwa nyara Jumamosi iliyopita alipokuwa akihudhuria hafla ya kuzinduliwa kwa kitabu cha Martha Karua. Ninafahamishwa kuwa anazuiliwa katika kambi moja ya kijeshi Jijini Kampala,” alisema Winnie.

Winnie alitoa wito kwa serikali ya Uganda kumuachilia huru mara moja kwa mume wake, akidai kuwa yeye si mwanajeshi.

“Mwachilieni huru mume wangu Dkt. Besigye  kutoka kule anakozuiliwa,” aliongeza Winnie.

Matamshi ya Winnie yanajiri baada ya vyombo vya habari nchini Uganda kuripoti kutoweka kwa Besigye, ambaye ni mkosoaji mkuu wa Rais Yoweri Museveni.

Share This Article