King Saha mwanamuziki wa Uganda alijipata pabaya pale ambapo alishambuliwa na mashabiki katika eneo moja ambapo alikuwa amealikwa kutumbuiza.
Saha alikuwa amealikwa katika mji wa Ibanda ambao uko katika eneo la Magharibi la Uganda kutumbuiza kwenye hafla ya kuzindua eneo moja na kuuza chakula na vinjwaji.
Punde alipoingia jukwaani, Saha alikabiliwa na tatizo la vifaa alivyokuwa akitumia huku akisema kwamba vilikuwa vibovu kuliko hata redio mbovu kwenye teksi.
Aliamua kuachana na ala za muziki na kuimba nyimbo zake huku akizungumza na watu ambao walikuwa wamekusanyika katika eneo hilo.
Usemi wake kuhusu siasa ndio ulimponza kwani wengi kati ya waliokuwepo walionekana kutokubaliana na maoni yake ya kisiasa.
“Mabadiliko yanakuja!!” alifoka mwanamuziki huyo ambaye anaaminika kuwa mfuasi sugu wa chama cha upinzani cha NUP akisahau kwamba eneo alilokuwa ni la watu wa chama tawala MRM.
Kimya kilijiri kwa sekunde kadhaa kabla yake kutupiwa chupa ambayo ilikuwa karibu kumgonga. “Ni nani huyo?” aliuliza mwanamuziki huyo na hapo ndipo alianza kutupiwa vitu vingi kama chupa, sahani za chakula na mabaki ya chakula.
King Saha aliondolewa jukwaani mara moja na ulinzi wake na sasa ameapa kuhakikisha anachagua vizuri maeneo ya kwenda kutumbuiza.