Waziri wa usalama wa taifa Profesa Kithure Kindiki amesema kwamba utoaji wa vifaa vya kazi kwa maafisa wa usalama walio katika maeneo muhimu kiusalama ni kati ya masuala yaliyopatiwa kipaumbele na serikali ya Kenya Kwanza.
Maeneo hayo ni pamoja na kaskazini mashariki, msitu wa Boni, mashariki ya juu na kaskazini mwa Rift Valley.
Kindiki alikuwa akizungumza leo wakati wa kuzindua vifaa vilivyonunuliwa kwa ajili ya kurahisisha kazi ya maafisa wa usalama katika maeneo husika.
Alisema serikali imejitolea kuangamiza kabiza ugaidi, ujambazi, wizi wa mifugo na aina nyingine za uhalifu uliopangwa, kama njia ya kubadili kabisa usalama wa kitaifa na kuiweka Kenya kwenye njia thabiti ya maendeleo sawia na ufanisi wa pamoja.
Waziri huyo alielezea kwamba katika muda wa miezi sita iliyopita, serikali imewekeza shilingi bilioni 7.6 na itatumia kiasi kingine cha shilingi bilioni 29.4 kwa muda wa miezi mitatu ijayo kwenye mpango wa kununulia maafisa wa usalama vifaa vya kisasa.
Vifaa hivyo ni pamoja na magari yasiyopenya risasi na yale ambayo hayaathiriwi na mabomu yanayotegwa chini ya ardhi, vifaa vya angani visivyodhibitiwa na binadamu kama droni, Helikopta za bunduki, vifaa vya kutegua mabomu na vifaa vya maafisa binafsi kujikinga wakiwa kazini.
Vifaa vilivyozinduliwa leo vinalenga kupiga jeki Oparesheni Maliza Uhalifu katika eneo la North Rift na vitatumika pia katika eneo la malisho ya mifugo kaskazini kaunti za Meru, Isiolo na Marsabit pamoja na eneo la Boni katika kaunti ya Lamu.
Katibu wa usalama wa taifa Raymond Omollo, Inspekta jenerali wa polisi Japhet Koome, manaibu wake Douglas Kanja na Noor Gabow, mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa jinai Mohamed Amin, kamanda wa kitengo cha GSU Eliud Lagat na maafisa wengine wa ngazi za juu katika huduma ya taifa ya polisi walishuhudia uzinduzi huo.