Waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki amesema kwamba usalama unaendelea kuimarika katika kaunti ya Turkana, kufuatia kuanzishwa kwa oparesheni ya “Maliza Uhalifu” mwaka mmoja uliopita.
Kindiki anasema kwamba mpango mzima wa usajili, mafunzo na kutumwa nyanjani kwa polisi zaidi wa akiba umesaidia sana katika kuimarisha usalama kupitia kupiga jeki juhudi za maafisa wengine wa usalama katika eneo hilo.
Anasema barabara kuu ya kutoka Kitale kuelekea Lodwar na maeneo mengine katika kaunti ya Turkana sasa ni salama.
Hata hivyo waziri Kindiki alisema kwamba bado wamesalia na jukumu la kukomesha mashambulizi yanayotekelezwa karibu na mpaka wa kaunti za Turkana na Pokot Magharibi.
Waziri Kindiki alifanya mkutano na kamati inayosimamia usalama na ujasusi katika mji wa Lodwar kaunti ya Turkana leo asubuhi ambapo alifahamishwa kuhusu hali ilivyo na wakajadili namna ya kukamilisha kazi ambayo imesalia.
Juma hili waziri Kindiki amekuwa akizuru kaunti mbali mbali ambapo amefanya mikutano na kamati za kaunti za usalama na ujasusi kujifahamisha kuhusu hali ilivyo.
Jana Jumatano, alizuru kaunti za Taita Taveta, Kwale, Mombasa, Kilifi na Tana River.