Naibu Rais Prof. Kithure kindiki amesema ujenzi wa daraja la Nithi utakaogharimu shilingi bilioni 7, utaanza katika muda wa wiki chache zijazo.
Kulingana na Kindiki, ujenzi wa daraja hilo utapunguza ajali za barabarani na kufanikisha shughuli za uchukuzi wa bidhaa na binadamu kwa njia salama.
Alidokeza kuwa kaunti ya Tharaka Nithi pia itanufaika na ujenzi wa kilomita 412 za barabara kwa shilingi bilioni 21 na mpango wa uunganishaji umeme kwa makazi kwa kitita cha shilingi bilioni moja kutoka kwa serikali ya taifa.
Aidha Prof. kindiki alisema nyumba za gharama nafuu, masoko ya kisasa na makazi ya wanafunzi, zitajengwa katika kaunti hiyo.
Kuhusu usajili katika mpango wa afya wa Taifa Care, kaunti ya Tharaka Nithi, ni miongoni mwa kaunti tano bora hapa nchini ambazo zimesajiliwa, na hivyo kuhakikisha kila mkenya anapata huduma bora za afya kwa bei nafuu.
“Asilimia 70 ya wakazi wa Tharaka Nithi wamesajiliwa katika mpango huo wa afya, ambao kufikia sasa umewasajili wakenya milioni 30.2, ikilinganishwa na wakenya milioni 7 waliokuwa wamesajiliwa kwenye mpango wa NHIF,” alisema Prof. Kindiki.
Kindiki aliyasema hayo Jumatano alipokagua miradi ya maendeleo katika eneo bunge la Chuka Igamba Ng’ombe, kaunti ya Tharaka Nithi.
Naibu huyo wa Rais alikuwa ameandamana na Gavana wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki, Naibu Gavana Nyaga Muisiraeli, Mwakilishi mwanamke Susan Ngugi, Wabunge Patrick Munene ( Chuka Igamba Ng’ombe), Kareke Mbiuki (Maara), Spika wa bunge la kaunti hiyo John Mbabu na wawakilishi wadi miongoni mwa viongozi wengine.