Kindiki: Serikali kuongeza uwekezaji eneo la Pwani

Kindiki amesema serikali inanuia kutekekleza maendeleo sawa katika kila pembe ya Kenya bila kujali miegemeo ya kisiasa, kabila au dini.

Tom Mathinji
1 Min Read

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amesema serikali inalenga kuongeza uwekezaji wa miundombinu na kuimarisha utoaji wa huduma muhimu katika eneo la Pwani ili kukabiliana na dhana ya kutengwa kwa eneo hilo kihistoria.

Akizungumza jana Jumanne alipokuwa akizindua uunganishaji umeme katika eneo la Kiruku, Lunga Lunga, kaunti ya Kwale, Kindiki alidokeza kuwa serikali ya Rais William Ruto itatenga fedha za kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara, uunganishaji umeme, maji, elimu, afya na huduma zingine ili kuhakikisha usawa kote nchini.

Kulingana na Naibu huyo wa Rais, kupitia kauli mbiyu ya Usawa ni Sawa, serikali inanuia kutekekleza maendeleo sawa katika kila pembe ya Kenya bila kujali miegemeo ya kisiasa, kabila, au dini.

Aliongeza kuwa mpango wa kusambaza umeme mashinani pia unaendelea katika vijiji jirani vya Kifuku na Mabandari na kwamba takriban nyumba 15,300 katika kaunti nzima ya Kwale zitaunganishwa umeme kwa gharama ya shilingi bilioni 1.8.

“Nyumba 15,300 katika kaunti ya Kwale zinaunganishiwa umeme kwa kitita cha shilingi bilioni 1.8,” alisema Kindiki.

Share This Article