Obado na wenzake kuhukumiwa leo Jumatano

Hii ni baada ya washtakiwa kupatikana na hatia Julai 23 katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno.

Martin Mwanje
2 Min Read

Gavana wa zamani wa kaunti ya Migori Zachary Okoth Obado na washtakiwa wenzake wawili watahukumiwa leo Jumatano baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno.

Uamuzi kuhusu kesi hiyo iliyofuatiliwa mno na umma ulitolewa Julai 23 na Jaji wa Mahakama Kuu Cecilia Githua.

Kwenye uamuzi wake, Jaji Githua alisema mahakama iliridhika na ushahidi uliowasilishwa uliothibitisha pasi na shaka kwamba watatu hao pamoja na wengine ambao hawakuwa mahakamani walishirikiana katika kutekeleza mauaji hayo.

Mshatakiwa wa kwanza Obado alilaumiwa kwa kuja na wazo la uovu huo, mshtakiwa wa pili Michael Oyamo akawezesha utekelezaji na mshtakiwa wa tatu Casper Ojwang akatoa usaidizi katika utekelezaji huo.

Kulingana na mahakama, kutokuwepo kwa mshtakiwa wa kwanza binafsi katika eneo la tukio siku hiyo, haikuwa sababu tosha ya kumpa kinga dhidi ya wajibu katika kesi hiyo ya jinai.

Jaji Githua alisema kwamba wajibu wa jinai hautegemei eneo ambalo watu walio na nia moja wapo.

Mahakama ilihitimisha kwamba mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu ni wahalifu wakuu kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha Kanuni ya Adhabu.

“Kwa kuzingatia ushahidi wa mazingira, washtakiwa hao walisababisha moja kwa moja kifo cha marehemu wakiwa na nia mbaya ya awali,” alisema Jaji huyo kwenye uamuzi wake.

Aliongeza kwamba upande wa mashtaka ulithibitisha kesi yake dhidi ya kila mmoja wa washtakiwa na hivyo, kila mmoja wao ana hatia kwa kosa hilo kama lilivyo katika hati ya mashtaka.

Share This Article