Serikali imesema itakabiliana vilivyo na visa vyovyote vya uhalifu huku ikiwalenga wafadhili na wanaochochea ghasia wakati wa maandamano yanayoendelea nchini.
Waziri wa Usalama wa Taifa Prof. Kithure Kindiki kupitia kwa taarifa leo Jumanne, alilaani ghasia zilizoshuhudiwa kote nchini, akidokeza kuwa mali ya mabilioni ya fedha iliharibiwa au kuporwa huku shughuli za uchukuzi zikitatizwa katika baadhi ya maeneo.
“Makundi ya wahalifu yameendelea kuhatarisha usalama wa umma kwa kuchoma mali, kutatiza uchukuzi wa umma na kuwashambulia wananchi,” alisema waziri huyo.
Taarifa yake inakuja baada ya ghasia kuzuka huku uporaji wa mali ukishuhudiwa katika sehemu mbalimbali za nchi wakati wa maandamano yaliyopangwa dhidi ya serikali.
Aidha, waziri aliwapongeza maafisa wa usalama kwa kudumisha utaalam wao wakati wa kukabiliana na waandamanaji.
“Serikali inawapongeza maafisa wote wa usalama ambao wanatekeleza wajibu wao wa kuzuia uhalifu na kulinda mali na maisha ya watu wa Kenya.”
Prof. Kindiki alisikitika kuwa, maandamano yangali yanaandaliwa licha ya Rais William Ruto kutangaza kuwa hatatia saini Mswada wa Fedha 2024.