Waziri wa Mambo ya Ndani Prof. Kithure Kindiki amefafanua kwamba polisi wa Kenya watatumwa nchini Haiti iwapo tu bunge litaidhinisha.
Akizungumza jana katika kanisa la St. Andrew ACK Ndenderu, eneo bunge la Kiambaa kaunti ya Kiambu, Kindiki alisema hakutakuwa na njia za mkato au ukiukaji wa katiba katika mchakato mzima wa kutuma kikosi cha polisi cha Kenya nchini Haiti.
Waziri Kindiki alielezea kwamba kifungu nambari 240 cha katiba ya Kenya kinaelekeza kwamba bunge ni lazima liidhinishe kutumwa kwa maafisa wa usalama kwenye nchi nyingine kudumisha usalama.
Huku akitoa mfano wa nchi za Namibia, Sierra Leone, Liberia, Somalia na Congo ambako Kenya imewahi kutuma maafisa wa usalama, Kindiki alisema kupelekwa kwa maafisa wa polisi nchini Haiti hakutahujumu kwa vyovyote kujitolea na kuwajibika kwa serikali kuhakikisha usalama wa wananchi.
Kuhusu ukosefu wa usalama katika kaunti ya Lamu, Kindiki alisema serikali imetambua wanaopanga na kuongoza utekelezaji wa visa vya ujambazi wakitumia visingizio vya dini na maovu ya jadi kuua wananchi ambao hawana hatia.
Waziri huyo alisema orodha ya majina ya washukiwa itatolewa wiki hii na ni lazima wajisalimishe kwa vituo vya polisi vilivyo karibu nao.
Katika kaunti za Kiambu na Murang’a, Waziri Kindiki alielekeza maafisa wa usalama kufunga maeneo yote yanayotumiwa na watu ambao alisema wanajificha kwenye utamaduni na kushambulia na kupotosha wananchi.