Serikali imeunda kamati itakayoratibu mipango ya mazishi ya kinara wa chama cha ODM Raila Odinga.
Odinga, alithibitishwa kufariki leo Jumatano wakati akipokea matibabu nchini India.
Kamati ya kupanga mazishi ya marehemu itaongozwa na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na Seneta wa Siaya Oburu Oginga.
Ujumbe wa kuurejesha mwili wa Raila kutoka India utaondoka nchini leo Jumatano.
Ujumbe huo utaongozwa na Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi.
Utajumuisha maafisa wa serikali na wanafamilia wa mwenda zake.
Upande wa familia unajumuisha mkewe Raila, Ida Odinga, Jaoko Oburu Odinga, Kevin Opiyo Oginga na wengineo.
Maafisa wa serikali wanajumuisha Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen na mwenzake wa Madini Hassan Joho, kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah na kiongozi wa walio wachache Junet Mohamed.
Nyumbani kwake Raila huko Bondo, wakazi walijitokeza kwa wingi kuomboleza kifo cha kiongozi wao waliyemuenzi kwa miongo kadhaa.
Hali ilikuwa vivyo hivyo katika maeneo mengi ya nchi.
Raila amefariki akiwa na umri wa miaka 80.