Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki amefichua kuwa takriban maduka elfu 18,650 ya kuuza pombe yamefungwa kote nchini kufikia sasa kwenye msako unaoendelea wa kukabiliana na pombe haramu.
Akizungumza alipozuru gereza la Kisii leo Jumatatu, Prof. Kindiki alisema kuwa serikali imefunga maeneo 12,150 ambayo yanahudumu bila leseni rasmi na mengine 6,500 yaliyo na leseni rasmi ila hayafuati sheria ya udhibiti wa pombe ya mwaka wa 2010.
Waziri alibainisha kuwa wamefunga maeneo 14 ya kutengeneza pombe ambayo yalikuwa yakihudumu kinyume cha sheria na kuharibu vifaa vya kutengeneza pombe hiyo.
“Pia tumefunga viwanda vingi vya kilimo na kemia vinavyofanya kazi kinyume cha sheria na tunafanya kazi kwa karibu na Bodi ya Famasia na Sumu (PPB) ambayo ndiyo wasimamizi wa sekta hiyo,” alisema.
Waziri huyo aliongeza kuwa washukiwa 95 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani katika kaunti ya Kisii.
Alidokeza kuwa serikali haitalegea katika juhudi zake za kuendeleza vita dhidi ya pombe haramu na matumizi ya dawa za kulevya hadi tatizo hilo litatuliwe kabisa.
Alikashifu athari za vileo na dawa za kulevya zenye sumu na zisizofaa kwa vijana akisema kuwa zimechangia viwango vya juu vya uhalifu nchini.
“Tangu tuanze msako huo kitaifa Machi 7, kumekuwa na kupungua kwa kasi kwa takwimu za uhalifu zilizoripotiwa kote nchini, ikimaanisha kuna uhusiano kati ya tatizo la pombe haramu na dawa za kulevya na viwango vya uhalifu,” Prof. Kindiki alisema.
Msako mkali unaoendelea wa kitaifa unafuatia agizo lililotolewa Machi 6 na Prof. Kindiki kuamuru kufungwa mara moja kwa baa na maduka ya pombe yanayofanya kazi katika maeneo ya makazi na karibu na taasisi za elimu.
Agizo hilo linajiri baada ya kisa cha kusikitisha kutokea Mwea Mashariki katika Kaunti ya Kirinyaga, ambapo watu 23 walifariki baada ya kunywa pombe haramu.