Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amesifia uhusiano ambao umeshamiri kati ya Kenya na China kwa kipindi cha miaka 61 iliyopita.
Prof. Kindiki amesema kupitia ushirikiano huo, hatua kubwa zimepigwa katika ufadhili wa miradi ya miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupitia mpango wa Ukanda Mmoja Njia Moja na Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, FOCAC.
“Wakati wa kipindi hiki, urafiki wa Watu hadi Watu na Serikali hadi Serikali umekua kwa mapana na marefu,” alisema Naibu Rais alipotembelewa katika makazi yake mtaani Karen na Balozi wa China Zhou Pingjian anayeondoka baada ya kukamilisha kipindi chake cha miaka minne ya kuhudumu humu nchini.
“Huku Balozi Pingjian akiondoka Nairobi baada ya kukamilisha muhula wake, Kenya inatafuta njia zaidi za kushirikiana na China kwa ajili ya ustawi wa watu wa nchi zote mbili.”