Kindiki azuru tena Nyayo House, amulika utaratibu wa utoaji pasipoti

Martin Mwanje
2 Min Read
Waziri Kindiki alipotembelea jumba la Nyayo leo Jumatatu asubuhi

Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki kwa mara nyingine alizuru jumba la Nyayo mapema leo Jumatatu kukadiria utekelezaji wa mabadiliko yanayolenga kuboresha na kuharakisha mchakato wa utoaji pasipoti. 

Wakenya wanaohitaji cheti hicho muhimu cha usafiri wamekuwa wakilalamika namna wanavyohangaishwa kupata stakabadhi hiyo, na nyakati nyingine baadhi kuitishwa mlungula.

Waziri Kindiki ameapa kuwaangamiza wafisadi wanaotatiza kuharakishwa kwa mchakato wa utoaji pasipoti na kuongoza ununuaji wa mashine zaidi za kuchapisha stakabadhi hiyo ili kuharakisha uchapishaji wake.

Maafisa wa uhamiaji nao wametakiwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mrundiko wa maombi ya pasipoti 40,000 unashughulikiwa chini ya siku 10 huku mipango ya kuajiri maafisa zaidi wa uhamiaji ikiwa imewekwa.

“Kuendeleza ari ya mabadiliko makubwa ili kuboresha utendakazi, kuangamiza ufisadi na kumaliza rundo la maombi ya pasipoti linasalia lengo la serikali ambalo ni lazima lifikiwe,” alisema Kindiki baada ya kuzuru jumba la Nyayo leo Jumatatu.

“Mapema leo asubuhi, nilifanya mkutano wa kuangazia hatua iliyopigwa, kufuatiilia na kutathmini mchakato wa utoaji pasipoti na maafisa wakuu wa Idara ya Uhamiaji wakiongozwa na Katibu wa Huduma za Uhamiaji na Raia Prof. Julius Bitok na Mkurugenzi Mkuu wa Uhamiaji na Huduma za Raia Evelyn Cheluget na baadaye kutembea hapa na pale kutahmini mazingira yanayobadilika ya utendakazi kwa ajili ya utoaji wetu wa huduma.”

Share This Article