Kindiki avitaka vyombo va habari kuwajibika katika utendakazi wake

Martin Mwanje
2 Min Read
Prof. Kithure Kindiki - Naibu Rais

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki ametoa wito kwa vyombo vya habari kuwajibika katika utendakazi wake kwa ajili ya manufaa ya maendeleo ya nchi. 

Hususan, Prof. Kindiki amevitaka vyombo vya habari kutoegemea upande wowote katika kuripoti yanayotendeka nchini.

“Tunatarajia kwamba hamtaegemea upande wowote katika kuripoti kwenu. Ingawa serikali siyo bora, ni muhimu pia kuangazia miradi ambayo inaleta mabadiliko chanya,” alisema Naibu Rais wakati akifungua rasmi Mkutano wa 7 wa kila Mwaka wa Chama cha Wahariri nchini (KEG) mjini Naivasha leo Ijumaa.

“Vyombo vya habari na serikali vinapaswa kupunguza tofauti zao kwa kukuza ushirikiano wa kikazi. Serikali inatambua wajibu muhimu unaotekelezwa na vyombo vya habari katika kuongoza ajenda ya umma na itaendelea kuunga mkono sekta hiyo.”

Kadhalika, Prof. Kindiki aliahidi kuwa serikali inashughulikia suala la madeni ambayo vyombo vya habari vinaidai serikali ili kuhakikisha vyombo hivyo vinaendelea kutekeleza majukumu yake itakikanavyo.

Ni wakati huo ambapo Naibu Rais alisema kuna haja ya kuimarisha utendakazi wa Shirika la Utangazaji nchini, KBC ili lihudumie umma vyema.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Dkt. Margaret Ndung’u aliahidi kushirikiana na vyombo vya habari katika kutumia teknolojia ili kukuza kwa njia chanya maendeleo ya jamii.

Wakati wa mkutano huo, Rais wa KEG Zubeida Kananu alitoa wito kwa vyombo vya habari kusimama kidete katika utendakazi wake kwa manufaa ya maendeleo ya jamii.

Kananu aliitaka serikali kuhakikisha usalama wa wanahabari, kuondoa maelekezo kandamizi ya matangazo ya biashara dhidi ya vyombo vya habari, kuunga mkono utendakazi wa vyombo vya habari na kuanzisha kituo cha taifa cha vyombo vya habari.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *