Kindiki asema UHC ni mpango jasiri na wenye athari kubwa

Alisema Wakenya milioni 32 sawa na asilimia 60 tayari wamejiandikisha na wanapata huduma chini ya mpango huu.

Marion Bosire
2 Min Read

Naibu Rais Kuthure Kindiki amesema kwamba mpango wa afya kwa wote ni mpango wa Kenya wenye ujasiri na athari zake ni kubwa ikilinganishwa na mipango mingine tangu Kenya kujipatia uhuru.

Kulingana naye, mpango huo unategemea nguzo tano ambazo ni wananchi, wataalamu sahihi wa afya, mfumo madhubuti wa kisheria, vifaa vya kisasa vya matibabu, pamoja na upatikanaji na usambazaji bora wa bidhaa za afya na huduma za usafirishaji.

Kuhusu wananchi, alisema Wakenya milioni 32 sawa na asilimia 60 tayari wamejiandikisha na wanapata huduma chini ya mpango huu.

Aliorodhesha hatua nyingine zilizopigwa chini ya mpango huo kama kuajiriwa kwa Wahamasishaji 107,000 wa Afya ya Jamii, madaktari wanaofanya mafunzo ya vitendo 24,000, madaktari bingwa wanaofanya usajili wa kitaalamu 282, pamoja na wauguzi na wakunga 5,000 watakaoajiriwa hivi karibuni, wanausukuma mpango huu kwa kasi isiyoweza kurejeshwa kuelekea siku zijazo.

Kiongozi huyo alitaja mpango wa Kitaifa wa Usaidizi wa Vifaa vya Tiba ambao tayari umeweka vifaa muhimu vya uchunguzi katika takribani vituo 239 vya afya vya ngazi ya 4 na 5, kwa gharama ya shilingi bilioni 9.8, kupitia utaratibu wa malipo kwa huduma zinazotolewa. Uwekaji wa vifaa vya msingi vya uchunguzi katika vituo vya afya vya ngazi ya 3 unaendelea.

Kingine alichokitaja Kindiki ni mfumo madhubuti wa kisheria ulioandaliwa kupitia Sheria ya Huduma ya Msingi ya Afya, Sheria ya Bima ya Afya ya Jamii, Sheria ya Afya ya Kidijitali na Sheria ya Ufadhili wa Uboreshaji wa Vituo vya Afya.

Sheria hizo alisema zimeanzisha taasisi mbili muhimu abazo ni Mamlaka ya Afya ya Jamii,SHA na Wakala wa Afya ya Kidijitali, DHA pamoja na mifuko minne mikuu: Mfuko wa Huduma ya Msingi ya Afya, Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii, Mfuko wa Dharura, Magonjwa Sugu na Magonjwa Mahututi, na Mfuko wa Uboreshaji wa Vituo vya Afya.

Share This Article