Kindiki azungumzia ombi la ulinzi la makundi ya usimamizi wa pamoja

Marion Bosire
2 Min Read
Waziri Kindiki katika kikao na kamati ya bunge kuhusu michezo na utamaduni

Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki amesema kwamba ombi la makundi ya usimamizi wa pamoja la kupatiwa ulinzi, wakati wa operesheni zao ni halali lakini ni lazima litekelezwe kupitia masikilizano na huduma ya taifa ya polisi.

Kindiki aliyasema haya alipokutana na kamati ya bunge la kitaifa kuhusu michezo na utamaduni kuzungumzia suala la makundi ya usimamizi wa pamoja la kupatiwa ulinzi na maafisa wa polisi wakati wa kutekeleza operesheni zao dhidi ya wanaokiuka sheria ya leseni za hakimiliki.

Ombi hilo lilitolewa na bodi ya kusimamia hakimiliki nchini, Kenya Copyright Board – KECOBO.

Ulinzi wa maafisa wa polisi kwa mashirika kama hayo uliondolewa mwaka 2020 wakati huduma ya taifa ya polisi ilionelea ni vyema itunze hadhi yake kutokana na ripoti nyingi za malalamiko kutoka kwa umma kuhusu visa vya maafisa wa makundi hayo kuwatoza hela baada ya kuwakamata na hatua ya makundi hayo kukosa kuwafikisha mahakamani waliokamatwa.

Waziri Kindiki anashikilia kwamba operesheni kama hizo ni lazima ziongozwe na makubaliano kuhusu mpangilio wa operesheni kama vile kumpa afisa wa polisi jukumu bayana ili kuhakikisha uwajibikaji.

Huduma ya Taifa ya Polisi ilisema itahakikisha utekelezaji wa sheria, ilinde haki ya wananchi ya kumiliki mali na kukamata wanaohujumu haki hizo.

Mashirika ya usimamizi wa pamoja ni kama yale ya kusimamia hakimiliki ya muziki ambayo mara kwa mara hutekeleza operesheni za kuhakikisha wanaotumia kazi za wasanii wanalipia kwa kupata leseni.

Share This Article