Kindiki afungua rasmi Kongamano la Biashara la COMESA

Martin Mwanje
2 Min Read

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amefungua rasmi Kongamano la Biashara la COMESA linalofanyika katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC, jijini Nairobi.

“Kongamano hili linawiana na ajenda ya mabadiliko ya kidijitali ya Kenya, ikitumia uongozi kinara wa kidijitali wa nchi katika teknonlojia ya utumaji na upokeaji pesa kwa njia ya simu, uongozi wa kidijitali na ubunifu wa Fintech,” alisema Naibu Rais wakati akizindua kongamano hilo.

“Ni lazima tuharakishe uendelezaji wa kilimo na mitungo mingine ya uongezaji thamani ya kikanda ni muhimu kwa mustakabali wetu. Sekta za umma na binafsi ni sharti zifanye kazi bega kwa bega kubini mazingira wezeshi ya kampuni kunawiri, kuwa bunifu na kupanuka.”

Kongamano la Biashara la COMESA linatoa fursa kwa eneo hili kukabiliana na changamoto za kibiashara.

Linateta pamoja wadau wa ngazi ya juu katika sekta binafsi, vyama mbalimbali, watoa huduma, washirika na sekta ya umma kujadili na kuidhinisha suluhu ambazo zitalichochea eneo la COMESA kuwa lenye uchumi wenye ushindani.

Akizungumza jana Jumatatu, Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe alidokeza kuwa serikali imeanzisha juhudi za kuhakikisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya kilimo, kuanzia shambani hadi sokoni.

Kagwe alitoa mfano wa mpango wa kitaifa wa ufuatiliaji wa shughuli mbalimbali za kilimo na uboreshaji wa taasisi za mafunzo ya kilimo, ili kuhakikisha uwazi kutoka shambani hadi sokoni na kuzingatia sera za mauzo ya nje.

Waziri huyo alitoa wito kwa Umoja wa Ulaya kushirikiana na Kenya katika kuboresha na kuzifanya taasisi za mafunzo ya kilimo kuwa za kisasa kwa kusudi la kuhakikisha  maafisa wa kilimo wa nyanjani wana vifaa vya kutosha siku zijazo.

Website |  + posts
Share This Article