Kikosi maalum cha usalama chapelekwa kurejesha utulivu Sondu

Tom Mathinji
1 Min Read
Ghasia zazuka katika mpaka wa Kaunti za Kisumu na Kericho. Picha/Hisani

Serikali imewahamisha maafisa wakuu wa usalama katika eneo la Sondu lililoko katika mpaka wa Kisumu na Kericho, ambalo limekumbwa na visa vya utovu wa usalama.

Hatua ya kuwahamisha maafisa hao wa usalama, imesababishwa na taharuki iliyoshuhudiwa kati ya jamii zinazoishi katika eneo hilo, pia itawaathiri maafisa wa umma ambao walitepetea kazini na kusababisha kutokea kwa uhalifu huo.

Akitangaza uhamisho huo wa maafisa wa usalama kupitia taarifa, waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki, alisema kikosi maalum cha maafisa wa usalama kimepelekwa kurejesha hali ya utulivu katika mji wa Sondu na viunga vyake.

“Kikosi hicho maalum kitakuwa chini ya kamati za usalama za maeneo ya Nyanza na Rift Valley, kikiwa na agizo la kurejesha hali ya utulivu, kuwakamata na kuwafungulia mashtaka waliohusika na uovu huo dhidi ya watu wa Sondu na viunga vyake,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kindiki alisema hatua zaidi za kudhibiti hali na kuzuia uhalifu katika eneo hilo, zitatangazwa.

Uhasama miongoni mwa jamii katika mpaka kati ya Kisumu na Kericho, umesababisha maafa, majeraha  na kuharibiwa kwa mali mapema wiki hii.

Share This Article