Kamanda mpya wa kikosi cha wanajeshi wa Kenya wanaohudumu katika Kikosi cha muungano wa Afrika cha kudumisha amani nchini Somalia (ATIMIS), Brigedia Seif Salim Rashid ameanza rasmi kazi akichukua mahali pa Brigedia William Kamoiro.
Wakati wa hafla ya kukabidhi majukumu hayo iliyoandaliwa katika makao makuu ya jeshi la ulinzi la Kenya (KDF) huko Dhobley, Brigedia anayeondoka alipongeza kikosi hicho kwa kukabiliana na Al-Shabaab na vikundi vingine haramu vilivyojihami katika maeneo walikotumwa.
“Wakati wa hatamu yangu tumetekeleza wajibu wetu kuambatana na mpango wa mpito wa Somalia,” alisema Brig. Kamoiro siku ya Jumanne.
Aliangazia kutuliza eneo la Jubaland na ulinzi wa raia kama mafanikio makubwa chini ya uongozi wake.
Kamanda huyo anayeondoka pia aliwasifu wanajeshi wa ATMIS, KDF kwa kuunga mkono mchakato wa mpito unaoongozwa na Somalia huku Brigedia Seif, akisisitiza ahadi yake ya kudumisha yaliyotekelezwa na mtangulizi wake.
Alitoa wito kwa wanajeshi kuendelea kuwa macho kwani kuna changamoto zinazoendelea za usalama na akaunga mkono wito wa mkuu wa majeshi ya Kenya (CDF), Jenerali Francis Ogola, wa umoja na azma ya kurejesha amani na utulivu katika kanda hii.