Kikao cha kujadili kubadilishwa kwa jina la City Mortuary chaahirishwa

Marion Bosire
2 Min Read

Kikao kilichokuwa kimepangwa cha kuwapa wakazi wa wadi ya Woodley/Kenyatta Golf Course katika kaunti ya Nairobi fursa ya kutoa maoni kuhusu kubadilishwa kwa jina la chumba cha kuhifadhi maiti cha “City Mortuary” kimeahirishwa.

Mwakilishi wa wadi hiyo Davidson Ngibuini maarufu kama DNG alitangaza hayo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii akitaja sababu ambazo hazingeweza kuepukika.

Awali kikao hicho kilikuwa kimepangiwa kuandaliwa Alhamisi Julai 4, 2024 lakini sasa anasema tarehe mpya ya kikao hicho itatangazwa baadaye.

Aprili mwaka 2023, Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja alitoa pendekezo la kubadili jina la makafani ya “City Mortuary” kuwa “Nairobi Funeral Home”.

Gavana Sakaja alitangaza hayo wakati alizuru eneo hilo lililo kwenye barabara ya Mbagathi, kukagua kazi iliyokuwa ikiendelea wakati huo ya kuliboresha.

Alifichua kwamba ukarabati ulikuwa ukiendelea humo na kwamba mabadiliko ya jina hilo ni njia ya kuhakikisha kwamba wanaofariki na miili yao kuhifadhiwa humo wanapata heshima wanayostahili.

Ukarabati na uboreshaji ulijumuisha kuweka vifaa vipya vya kuhifadhi maiti, milango mipya ya vyumba vya vifaa hivyo na uboreshaji wa mifereji ya kuondoa maji taka.

Mwaka 2021 mmoja wa wahudumu wa City Mortuary alifichua kwamba vifaa vya makafani hayo vilikuwa vibovu na ukarabati wake wa kila mara uligharimu pesa nyingi.

Afisa mkuu wa afya ya umma katika serikali ya kaunti ya Nairobi wakati huo Tom Nyakaba alijibu akisema walikuwa wametafuta mwanakandarasi wa kutekeleza ukarabati.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *