Kifungo cha miezi mitatu kwa mrembo wa Rwanda Divine Muheto

Marion Bosire
1 Min Read

Divine Muheto mshikilizi wa taji ya Miss Rwanda mwaka 2022 atatumikia kifungo cha miezi mitatu, hukumu iliyotolewa dhidi yake na mahakama ya Kicukiro nchini Rwanda.

Kifungo hicho cha nje ni adhabu kutokana na hatia aliyopatikana nayo ya kuendesha gari akiwa mlevi, bila leseni na kuharibu miundomsingi jijini Kigali.

Muheto anatakiwa pia kulipa faini ya faranga 190,000 za Rwanda sawa na shilingi elfu 18 za Kenya.

Mrembo huyo anahitajika kuhakikisha maadili ya kiwango cha juu katika muda wa miezi hiyo mitatu na iwapo atapatikana na kosa sawia ndani ya muda huo, basi atafungwa jela.

Alikaa rumande kwa siku 18 kabla ya kuachiliwa Jumatano Novemba 6, 2024 kufuatia amri iliyotolewa na jaji.

Oktoba 20,2024 ndiyo siku Muheto alikamatwa na polisi walikiri kwamba hiyo haikuwa mara ya kwanza kwake kutenda kosa sawa na hilo.

Shindano na Miss Rwanda lilipigwa marufuku kutokana na kile kinachosemekana kuwa ukosefu wa maadili kati ya waandalizi na hivyo Muheto anasalia kuwa Miss Rwanda hadi sasa.

Share This Article