Uchunguzi wa maiti ya mwanahabari Rita Tinina umebainisha kwamba alifariki kutokana na maradhi ya nimonia yaliyokolea.
Msemaji wa familia ya marehemu Tinina kwa jina Timothy Nyaga alishuhudia uchunguzi huo uliotekelezwa na Daktari Michaka. Familia ya marehemu imeelezea kuridhika na matokeo ya uchunguzi huo.
Tinina alipatikana amefariki katika makazi yake mtaani Kileleshwa kaunti ya Nairobi, habari ambazo zilishtua wengi.
Alikuwa anatarajiwa kufika kazini siku hiyo na wafanyakazi wenza walipojaribu kumtafuta kupitia kwa simu yake ya mkononi, hawakufanikiwa.
Taarifa kutoka kwa polisi kuhusu kifo cha Tinina ilielezea kwamba marehemu ambaye alikuwa mhariri wa taarifa za Kiingereza katika shirika la habari la Nation Media Group alikuwa anaugua kifafa na alikuwa na homa kali ambayo ilikuwa imedumu siku tano.
Familia ya Tinina inaomba umma kuwapa muda wa kuomboleza mpendwa wao.