Rais William Ruto ametangaza kipindi cha maombolezi ya kitaifa cha siku saba, kufuatia kifo cha kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.
Katika hotuba rasmi ya kutangaza kifo cha Raila kutoka Ikulu ya Nairobi, Rais alisema hatua hiyo ni ya kutambua mchango mkubwa wa Raila kwa taifa la Kenya.
Wakati wa maombolezi hayo, bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kote nchini na katika balozi za Kenya kimataifa, huku Rais akiahirisha shughuli zake zote kujumuika na wakenya katika maombolezi.
“Kama ishara ya heshima, nimeahirisha shughuli zangu zote za siku kadhaa zijazo ili kuungana na taifa katika maombolezi.” Alisema Rais katika hotuba hiyo.
Zaidi ya hayo Rais Ruto alielezea kwamba Odinga atapatiwa mazishi ya kitaifa pamoja na heshima zote.
Kiongozi wa nchi alitangaza pia kubuniwa kwa kamati ya maandalizi ya mazishi hayo baada ya mashauriano na familia ya Raila Odinga ambayo alizuru mapema leo huko Karen.
Naibu Rais Kithure Kindiki na kaka mkubwa wa Raila , Oburu Odinga ambaye ni Seneta wa kaunti ya Siaya watakuwa wenyeviti wenza wa kamati hiyo ya mazishi.
Kiongozi wa nchi alifahamisha taifa pia kwamba serikali ya India imekubali kusafirisha mwili wa Odinga hadi Kenya kufuatia ombi lililowasilishwa na serikali ya Kenya.
Kwa sababu hiyo, waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi anaongoza ujumbe wa viongozi mbali mbali kuelekea India leo kufanikisha usafirishaji huo.
Wanafamilia wa mwendazake pia wataelekea India pamoja na ujumbe huo kwa sababu hiyo akiwemo mjane Mama Ida na wanawe, Jaoko
Oburu Odinga, Kevin Opiyo Oginga na wengine.
Rais Ruto alimalizia kwa kuhimiza wakenya kuangazia kwa undani urithi wa mheshimiwa Raila Odinga na mafunzo ambayo yalitokana na maisha yake, kazi zake, mawazo yake na hata mwongozo.