Khaligraph Jones aingiana na utani kuhusu jumba lake

Marion Bosire
2 Min Read

Saa chache baada ya jumba lake kuzua minong’ono mitandaoni, mwanamuziki Khaligraph Jones ameamua kufuata mkondo wa utani mitandaoni unaohusu jumba lake.

Alichapisha picha inayomwonyesha akiwa kwenye sebule jumbani humo na kuandika, ” Habari za asubuhi, ninaripoti moja kwa moja kutoka garden city, tayari kupokea ushauri wenu kabla ya kuanza siku. OG ataheshimiwa.”

Wafuasi wake mitandaoni walifananisha jumba lake na jumba la kibiashara la Garden City Mall naye akaamua kuendana na utani wao.

Alipoalika wafuasi wake hadi nyumbani kwake kwa njia ya video, Jones ni kama alifahamu utani utakaofuata huku akijieleza akisema wakenya hawajazoea majumba kama hayo.

Jones anasema jumba lake linafanana na la mwanamuziki na mfanyabiashara wa Marekani Rick Ross.

Baadhi ya wafuasi wake mitandaoni walianza kuhariri picha za nyumba hiyo wakibandika mabango ya maduka tofauti yanayopatikana kwenye Garden City Mall.

Daddy Owen alimtetea Khali akishangaa wanachokata mashabiki wa Kenya. Alisema awali waliguna kwa sababu wasanii hawakuwa na pesa, sasa wana pesa lakini bado miguno ipo.

“Khaligraph amekuwa akionyesha mchakato wake wa kuimarika kutoka mtaa wa Kayole hadi kwenye jumba la mamilioni ya pesa. Ameonyesha kwamba unaweza kuafikia ndoto zako bila wizi, ukora ama washwash!” aliandika Daddy Owen.

Aliwataka mashabiki kukoma kukejeli bidii ya Khaligraph na badala yake kumuunga mkono hasa kwa sababu wameona jinsi alikua.

“khaligraph Jones ninajua mapambano yako, nilikuwepo hata kabla haujakuwa nyota na ninajua uliyoyapitia!” Owen alimhimiza Khali huku akitaka aheshimiwe na ashukuru Mungu huku akifurahia mibaraka.

Share This Article