Mwanasheria Mkuu Justin Muturi aliwasilisha mahakamani taarifa ya kupinga uamuzi wa mahakama kuu uliotolewa juzi Jumatatu na ambao ulibatilisha uteuzi wa nawaziri wasaidizi 50 uliotekelezwa na Rais William Ruto.
Kesi hiyo itatajwa leo saa tatu asubuhi na Jaji Mugure Thande.
Uamuzi huo uliotolewa na jopo la majaji watatu, ulibaini kwamba umma ulihusishwa katika uteuzi wa mawaziri wasaidizi 23 pekee na uteuzi wa wengine 27 haukutimiza mahitaji ya sheria.
Majaji walisema kwamba kutokana na rekodi walizokuwa nazo, tume ya utumishi wa umma ilikosa kutekeleza wajibu wake ipasavyo. Kulingana nao, gharama ya kutenga nafasi 27 zaidi za mawaziri wasaidizi ni kinyume cha katiba.
Majaji Kanyi Kimondo na Aleem Visram walisema kwamba haikuwa nia ya waandishi wa katiba kwamba kuwe na mawaziri wasaidizi 50 kuwasaidia mawaziri 22. Kwao, uteuzi wa wote 50 ulikuwa kinyume cha katiba.
Jaji Hedwig Ong’undi kwa upande wake alisema ni mawaziri wasaidizi 27 walioteuliwa kinyume cha sheria lakini 23 ni halali.
Awali, tume ya utumishi wa umma, wakati wa utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ilikuwa imetenga nafasi 23 za mawaziri wasaidizi.
Machi 16, 2023 Rais William Ruto aliteua mawaziri wasaidizi 50 huku nafasi zilizokuwepo zikiwa 23.
Hamsini hao waliapishwa Machi 23 baada ya bunge la kitaifa kukosa kuwasaili kwa sababu halikuwa na mamlaka.
Machi 24, mahakama kuu ilitoa agizo la kuwazuia wote 50 kuanza kazi na kupokea mishahara na marupurupu hadi kesi iliyowasilishwa na chama cha mawakili nchini, LSK na Katiba Institute isikilizwe na kuamuliwa.