Gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo amekubaliwa kuongoza timu ya wanasheria ya Bunge la Taifa wakati wa vikao vya Bunge la Seneti vya kusikiza mashtaka dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Timu ya wanasheria ya Gachagua ilikuwa imepinga Orengo kulikwakilisha Bunge la Taifa ikitaja kuwepo kwa mgongano wa maslahi ikizingatiwa Orengo ni afisa wa serikali.
Mwanasheria Ndegwa Njiru alisema kwa kuliakilisha Bunge la Taifa wakati wa vikao hivyo, Gavana Orengo atakuwa anajihusisha katika kazi anayonufaika nayo kimapato kinyume cha katiba.
Hata hivyo, mwanasheria Eric Gumbo alipinga msimamo wa upande wa timu ya wanasheria ya Naibu Rais akisema hakuna ushaihidi uliowasilishwa kudhihirisha kuwa Orengo alinufaika na malipo yoyote kwa kuliwakilisha Bunge la Taifa katika vikao hivyo.
Katika uamuzi wake, Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi alikubaliana na Gumbo. Kingi alisema hakuna ushahidi uliowasilishwa na upande wa Gachagua kudhihirisha kwamba Orengo alinufaika na malipo yoyote kwa kuliwakilisha Bunge la Taifa katika vikao hivyo vilivyoanza leo JUmatano.
Kwa misingi hiyo, Orengo hakukiuka katiba na hivyo ataendelea kuliwakilisha Bunge la Taifa katika vikao hivyo vitakavyoamua hatima ya Gachagua katika kuendelea kuhudumu kama Naibu Rais.