Kesi kuhusu mauaji ya Monica Kimani kuamuliwa Disemba 15

Tom Mathinji
1 Min Read
Jackie Maribe na Joshua Irungu, kujua hatma yao tarehe 15 Disemba.

Mahakama Kuu imeahirisha kutoa hukumu dhidi ya Joseph Irungu almaarufu Jowie na Jackie Maribe kufuatia mauaji ya mwanabiashara Monica Kimani yaliyotekelezwa mwezi Septemba mwaka 2018.

Mahakama hiyo sasa itatoa hukumu dhidi ya wawili hao tarehe 15 mwezi Disemba mwaka huu.

Jaji Grace Nzioka alitarajiwa kutoa hukumu hiyo leo Ijumaa, lakini akaahirisha, kwa kuwa anaugua.

Upande wa mashtaka uliwaita mashahidi 35, ambao walitoa ushahidi dhidi ya Jackie Maribe na Joseph Irungu.

Wakili wa upande wa mashtaka Gichui Gikui, alimwambia Jaji Grace Nzioka kuwa wawili hao walihusishwa na mauaji hayo ya kinyama ya Monica.

Alisema kuwa siku ambayo mauaji hayo yalitekelezwa, Irungu alionekana akiingia nyumbani kwa Monica, na akaelekea kubadilisha mavazi.

Kulingana na wakili huyo, Irungu alikuwa na bastola na kwamba Monica alifahamu hivyo.

Gikui alisema bunduki iliyotumiwa kutekeleza mauaji hayo, iliwasilishwa kotini na kwamba ripoti ya uchunguzi wa DNA iliashiria kuwa sampuli za damu kutoka kwa Jowie, ziliambatana na zile za Monica.

Hata hivyo, wakili wa Maribe Katwa Kigen, aliambia mahakama kwamba, upande wa mashtaka ulishindwa kutoa ushahidi kumhusisha mteja wake na mauaji hayo.

Kigen alisema siku ambayo Monica aliuawa, Jackie Maribe alikuwa kazini hadi saa sita usiku, kabla ya kujiunga mwanasiasa mmoja katika kituo kimoja cha burudani.

Share This Article