Kenya inaungana na mataifa mengine duniani leo Alhamisi, kuadhimisha siku ya afya ya akili ulimwenguni.
Maadhimisho hayo ya kila mwaka ya Oktoba 10, yalianzishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa lengo la kuangazia hali zisizofaa ikiwa ni pamoja na unyanyapaa, ubaguzi, na kuathiriwa na hatari kama vile unyanyasaji na mazingira mengine mabaya ya kazi ambayo yanaweza kusababisha hatari kubwa ya ki-akili.
Maadhimisho hayo yanaandaliwa huku Shirika la Afya Duniani litoa ripoti mpya kuwa mtoto mmoja kati ya saba walio na umri wa kati ya miaka 10 na 19, wanaathiriwa na matatizo ya akili.
Ripoti hiyo iliyotolewa siku ya Jumatano, aidha iliashiria kuwa thuluthi moja ya matatizo ya akili huathiri watoto kabla ya kutimia umri wa miaka 14 na nusu.
Kulingana na ripoti hiyo, ipo haja ya hatua za mapema kuchukuliwa kuhakikisha watoto na vijana wanatimiza kikamilifu malengo yao.
Huku hayo yakijiri, wadau wa afya hapa nchini wamesema kuwa wanaoathiriwa na matatizo ya akili wametelekezwa na wanateseka kutokana na itikadi potovu.
Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza katika kaunti ya Siaya, Peter Omoth, alisema juhudi madhubuti zinafaa kufanywa ili kudhibiti tatizo la afya ya akili.