Rais William Ruto amepata mkopo wa maendeleo wa dola milioni 485 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 63 za Kenya kutoka kwa Jamhuri ya Korea Kusini.
Mkopo huo unajumuisha dola milioni 238 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 30.9 kwa ajili ya Mradi wa Jiji la Teknolojia ya Konza.
Kulingana na Rais Ruto, ambaye amefanya mazungumzo na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol, kituo hicho kipya kitaimarisha mfumo wa kidijitali humu nchini na kupanua fursa kwa vijana katika uchumi bunifu.
Ruto yuko nchini Korea Kusini akihudhuria Kongamano la Korea na Afrika.
Kongamano hilo linafanyika katika Kituo cha Maonyesho cha Kimataifa cha Korea mjini Goyang viungani mwa mji mkuu wa Seoul.
Mazungumzo kati ya Marais hao yalijadili hali ya ushirikiano wa shilingi za Kenya bilioni 132 za Mpango wa Mfumo ambao ulikubaliwa wakati wa ziara yake ya awali mnamo mwezi Novemba mwaka 2022. Kulingana na msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed, majadiliano ya siku ya Jumapili ijayo kati yao yatahusu tija ya kilimo, mwitikio wa mabadiliko ya hali ya tabia nchi na mpito kwa nishati isiyo na kaboni.
Aliongeza kuwa viongozi hao kadhalika watakamilisha makubaliano ya thamani ya shilingi bilioni 40 ili kuunda fursa katika sekta ya uchumi bunifu wa Kenya na shilingi bilioni 25 kwa miradi ya maji na umwagiliaji.
Hussein alifuchua kuwa mikataba kadhaa ya maelewano pia itatiwa saini ili kuimarisha ushirikiano katika afya, kilimo na teknolojia na mawasiliano kati ya sekta nyingine. Alisema Kenya itashirikisha Korea Kusini katika kuchunguza fursa za teknolojia, ikiwa ni pamoja na kuendeleza sekta yake ya semikondakta.
Kenya pia itajiunga na Taasisi ya Kimataifa ya Chanjo (IVI) ili kuendeleza malengo yake ya utengenezaji wa chanjo.
Kenya na Korea Kusini zinatarajiwa kukamilisha Mpango wa Uhamiaji wa Wafanyakazi, uwezekano wa kuifanya Kenya kuwa miongoni mwa nchi chache za Kiafrika zilizoidhinishwa kwa usambazaji wa vibarua chini ya Mpango wa Mfumo wa Kibali cha Ajira cha Korea Kusini (EPS).
Mataifa hayo mawili pia yanakusudia kuanzisha mazungumzo ya Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi baina yao.