Kenya imependekeza kuondoa ushuru wa mayai, viazi na vitunguu kwa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC kama njia ya kuinua biashara miongoni mwa mataifa wanachama.
Waziri wa Fedha Prof. Njuguna Ndung’u alipendekeza kuondoa ushuru wa forodha wa asilimia 25, uliokuwa umewekwa kwa bidhaa hizo, hatua ambayo ilikuwa imedumaza biashara kati ya mataifa wanachama wa EAC.
Ushuru huo wa forodha uliondolewa kufuatia mashauriano kati ya Rais William Ruto na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni. Mayai mengi huingizwa humu nchini kutoka Uganda.
Kuondoa ushuru wa forodha kwa viazi na vitunguu kunatarajiwa kupunguza bei ya bidhaa hizo, iliyokuwa imeongezeka kwa asilimia 67.7 kwa kilo ya vitunguu, huku ile ya viazi ikipanda kwa asilimia 10.
Ushuru wa bidhaa za chuma kutoka EAC umeongezwa kutoka asilimia 25 hadi 35 kulingana na bajeti iliyosomwa na Prof. Ndungu, huku vyakula vya mifugo vikisalia bila ushuru, nao ushuru wa forodha kwa bidhaa za ngozi kutoka EAC ukipandishwa kutoka asilimia 25 hadi 35.