Kenya imeitisha usaidizi wa kiufundi na kifedha kutoka kwa Brazil, ili kuimarisha juhudi za kuleta amani nchini Haiti.
Ombi hilo linajiri siku chache baada ya waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi ambaye yuko kwenye ziara rasmi nchini Brazil, kuitaka jamii ya kimataifa kutumizi na kuongeza ufadhili kwa mpango huo wa kiusalama unaoongozwa na Umoja wa Mataifa.
Mudavadi aliyepia waziri wa Mambo ya Nje, aliitisha usaidizi huo wa Brazil, alipokutana na mwenzake wa Brazil balozi Mauro Vieira afisini mwake Jijini Brasilia wakati wa mkutano wa 5 kuhusu mashauriano ya kisiasa kati ya Kenya na Brazil.
“Nilimfahamisha waziri Vieira kuhusu juhudi za kiusalama za kuleta amani nchini Brazil na kuitisha usaidizi wa kiufundi na kifedha kutoka taifa lake kufanikisha juhudi za kuleta amani nchini Haiti,” alisema Mudavadi.
Mudavadi, alisema Kenya na Brazil zimejitolea kuboresha uhusiano wa pande mbili kwa manufaa ya raia wa mataifa hayo mawili.
“Tunarejelea kujitolea kwetu kuboresha uhusiano wa nchi hizi mbili kwa kutia saini Mkataba wa Maelewano kuhusu Utalii. Mazungumzo yetu pia yaliangazia fursa zilizopo za ushirikiano zaidi katika sekta za Kilimo, Biashara,Afya, Mabadiliko ya Tabia Nchi na Usalama,” alidokeza Mudavadi.
Katika ziara hiyo, Mudavadi ameandamana na balozi wa Kenya nchini Brazil Dkt. Andrew Karanja, na balozi Lucy Kiruthu, kaimu Mkurugenzi Mkuu wa maswala ya siasa na diplomasia.
Kabla ya kuelekea Brazil, Mudavadi alifanya ziara katika Jamhuri ya Dominican, ambako alishauriana na Waziri wa Mambo ya Nje Roberto Álvarez Jijini Santo Domingo siku ya Jumanne.
Kenya imewapeleka maafisa 800 wa polisi kusaidia kurejesha hali ya usalama nchini Haiti. Hadi kufikia sasa maafisa wawili wa polisi wamefariki na kadhaa wamejeruhiwa, wakikabiliana na makundi ya magenge nchini humo.