Kenya yahofu kufuatia kuzuiliwa kwa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini

Martin Mwanje
2 Min Read
Musalia Mudavadi - Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje

Kenya imeelezea mashaka kuhusiana na hali ilivyo nchini Sudan Kusini, hasa kutokana na ripoti kwamba Makamu wa Rais wa Kwanza wa nchi hiyo Dkt. Riek Machar alizuiliwa nyumbani kwake jana Jumatano usiku. 

Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi sasa anatoa wito kwa pande husika katika mzozo unaorindima nchini humo kuwa mstari wa mbele kutafuta amani ya kudumu.

“Serikali ya Kenya inatoa wito kwa pande zote nchini Sudan Kusini kutoa kipaumbele nchini humo kwa kutoa nafasi kwa makubaliano ya amani yanayoendelea chini ya mwavuli wa Makubaliano ya Uhuishaji ya IGAD juu ya Utatuzi wa Mgogoro katika Jamhuri ya Sudan Kusini (R-ARCSS),” alisema Mudavadi kwenye taarifa iliyotolewa leo Alhamisi.

“Tunatoa wito kwa viongozi wote wa Sudan Kusini kujizuia mno, kusitisha uhasama, na kuheshimu Makubaliano ya Amani Yaliyohuishwa kwa maslahi bora ya mamilioni ya watu wao,” aliongeza Mudavadi ambaye pia ni Mkuu wa Mawaziri.

Chama cha Dkt. Machar cha Sudan People’s Liberation Movement (SPLM/IO) kimesema Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini amewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani.

Kiliongeza kuwa msafara wenye silaha ukiongozwa na maafisa wakuu wa usalama uliingia katika makazi ya Machar katika mji mkuu, Juba, na kuwanyang’anya walinzi wake.

Dkt. Machar ni mpinzani wa muda mrefu wa Rais wa nchi hiyo Salva Kiir.

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *