Kenya imefaidi pakubwa kutokana na kongamano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, COP28 linaloendelea jijini Dubai katika Ufalme wa Milki za Kiarabu, UAE.
Kenya imetia saini mikataba kadhaa ya uwekezaji katika nishati safi baada ya Rais William Ruto kuongoza viongozi wengine wa bara Afrika katika mikutano ya mpango wa Afrika wa viwanda visivyochafua mazingira.
Mikutano hiyo ilichochea kupatikana kwa dola bilioni 1.5 za Marekani na kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 225 zitatumika kufadhili miradi ya kutengeneza mbolea.
Bilioni 90 zimetengewa kituo cha data ambacho kitaundwa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya KenGen na Konza City huku shilingi bilioni 150 zikiwekezwa katika mradi wa kuzalisha umeme kutokana na mvuke wa ardhini katika eneo la Suswa.
Rais Ruto ameelekea India kwa ziara rasmi ya siku 2 baada ya kuhudhuria kongamano la COP28.