Timu ya taifa ya Kenya ya raga kwa wanaume saba upande -Shujaa, imeanza michezo ya Olimpiki ndivyo sivyo baada ya kuambulia kipigo cha kitutu cha pointi 31-12, kutoka kwa Argentina, katika mchuano wa kundi B Jumatano jioni jijini Paris Ufaransa.
Chrisant Ojwang alipachika try ya kwanza ya Kenya dakika ya 4, kabla ya Anthony Mboya kuongeza pointi 2 kupitia Conversion.
Agustin Fraga alikomboa try kwa Argentine katika dakika ya mwisho kipindi cha kwanza huku Kenya ikiongoza alama 7-5 kufikia mapumziko.
Argentina walirejea kipindi cha pili kwa matao ya juu Fraga akiongeza try ya dakika ya 8 naye Joaquin Pellandini akafunga conversion na kuwaweka Waamerika hao uongonzini alama 12-7.
Kevin Wekesa aliisawazishia Kenya katika dakika ya 9 mambo yakiwa sahani na kawa 12-12.
Utepetevu wa Shujaa uliwapa fursa Tomas Ezilade,Rizzoni Gonzales na Marcos Moneta kupachika try moja kila mmoja, nao Mare na Pellandini wakaongeza alama 2 kila mmoja kuhawakikishia Argentina ushindi wa 31-12.