Kenya yaandaa mkutano wa kanda wa kupambana na silaha haramu

Marion Bosire
2 Min Read

Katibu wa Usalama wa Taifa Raymond Omollo leo alizindua rasmi mkutano wa wataalamu wa silaha ndogo jijini Nairobi.

Mktano huo unawaleta pamoja wadau wa eneo hili ili wabuni mikakati ya kiushirikiano kwa lengo la kumaliza kuenea kwa silaha ndogo haramu, suala linalohatarisha amani na usalama wa eneo hili.

Omollo alingana na Jean Pierre Betindji, ambaye ni katibu mtendaji wa kituo cha eneo hili cha silaha ndogo – RECSA na Jacinta Muthoni mkurugenzi wa shirika la kitaifa kuhusu kitovu cha silaha ndogo -KNFP.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Dr. Omollo alisisitiza haja ya kuimarisha usimamizi wa mipaka, kuimarisha mifumo ya kisheria na kuhimiza usafirishaji unaofaa wa silaha ili kukabiliana na tatizo lililopo.

Aliangazia pia haja ya kuboresha usimamizi wa hifadhi ya silaha hizo na utekelezaji wa shughuli za kupokonya watu silaha haramu, mipango ya kusambaratisha na kuunganisha tena na jamii kwa lengo la kukuza maisha yenye amani na tija.

“Kupitia kwa juhudi za pamoja, tunaweza kupiga hatua kubwa katika kupunguza upatikanaji wa silaha haramu na kupunguza athari zake mbaya.” alisema katibu Omollo.

Akigusia hatua zilizopigwa tangu kubuniwa kwa RECSA mwaka 2005, Omollo alitambua maendeleo yaliyopatikana katika kushughulikia biashara ya silaha haramu na uimarishaji wa mifumo ya kitaifa ya usalama kati ya nchi wanachama.

Omollo alisisitiza kujitolea kwa Kenya kwa ushirikiano wa kikanda katika kushinda changamoto hizi na akahimiza juhudi zaidi katika kuendeleza yaliyoafikiwa hadi sasa.

Share This Article