Waziri wa mazingira Aden Duale, leo Alhamisi atawaongoza wakenya kuadhimisha siku kuu ya Mazingira katika bustani ya Arboretum Jijini Nairobi.
Waziri huyo ametoa wito kwa wakenya kushiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira kama vile upanzi wa miche pamoja na shughuli nyingine za usafi katika jamii zao kwa ajili ya siku ya Mazingira ya mwaka huu itakayoadhimishwa hapo kesho.
Duale aliwataka wakenya kuhakikisha mazingira wanamoishi ni safi, kwa kutekeleza katika fuo, bustani, nyumbani na maeneo mengine.

“Wakenya wanahimizwa kujihusisha na uhifadhi wa mazingira katika maeneo wanamoishi, ikiwa ni pamoja na upanzi wa miche na shughuli zingine za usafi ili kuadhimisha siku hii,” alisema Duale kupitia taarifa.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza Kenya kuadhimisha siku ya Mazingira tarehe 10 mwezi Oktoba.
Hapo awali siku hii ilijulikana Moi Day, kabla ya kubadilishwa jina kuwa Huduma Day, baadaye Utamaduni Day na hatimaye Mazingira Day.
Sherehe hizo za kitaifa zitaandaliwa katika bustani ya Arboretum.