Kenya na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, UNDP zimetia saini Makubaliano ya Maelewano ambapo UNDP itasaidia nchi hiyo katika uzinduzi uliopangwa wa kitambulisho cha kidijitali.
Chini ya makubaliano hayo, UNDP itatoa usaidizi wa kiufundi na kufanya kazi na serikali kuchangisha fedha na rasilimali zingine ili kuunga mkono uendelezaji na utekelezaji wa kitambulisho hicho.
Katibu wa Uhamiaji na Huduma za Raia Prof. Julius Bitok na Anthony Ngororano ambaye ni Mwakilishi Mkazi wa UNDP walisaini makubaliano hayo kwa niaba ya serikali na shirika hilo la Umoja wa Mataifa, UN mtawalia.
Kulingana nao, ushirikiano huo pia utahusisha ufuatiliaji wa uzinduzi wa kitambulisho cha kidijitali.
“Huu ni mradi muhimu na hiyo ndio sababu tunatumia ushirikiano na ushauri wa kiufundi kutoka kwa UNDP kuafikia kitambulisho thabiti cha kidijitali,” alisema Prof. Bitok.
Aliongeza kuwa Kenya inatumai kunufaika kutokana na tajiriba pana ya UN iliyopatikana kwa kuzisaidia nchi zisizopungua 25 kote duniani kuendeleza mifumo yao yenyewe ya kitambulisho cha kidijitali.
Uzinduaji wa kitambulisho cha kidijitali pia unalenga kuifanya Kenya kutii viwango vya kimataifa vya usafiri wa kuvuka mipaka vilivyowekwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga, ICAO na mashirika mengine.
Kwa upande wake, Ngororano alielezea kitambulisho cha kidigitali kuwa kiunganisho kinachokosekana kati ya raia na upatikanaji wa huduma za kidijitali akiongeza kuwa UNDP inadhamiria kuiunga mkono serikali kuziba pengo hilo.
Wakati wa utiaji saini huo, Katibu Bitok alisema serikali ilijifunza mengi kutokana na changamoto za awali katika utekelezaji wa miradi sawia.
Alidokeza kuwa serikali itazindua bidhaa zingine nne husika kuendana na agizo la rais ili kuunda kitambulisho cha kidijitali.
Bidhaa hizo ni maisha namba, kadi ya maisha, kitambulisho cha kidijitali na sajili kuu ya kitaifa ya watu.