Baada ya kufeli mara mbili, hatimaye Kenya iko tayari kuandaa kipute cha soka kikubwa Afrika, mashindano ya kuwania kombe la CHAN.
Kenya itakuwa mwenyeji wa fainali za CHAN, mashindano ya soka yanayoshirikisha wachezaji wa ligi za nyumbani kuanzia Jumamosi hii, Agosti 2-30.
Ni mara ya pili katika historia kwa Kenya kupewa maandalizi ya kipute hicho baada ya kutwikwa jukumu hilo mwaka 2018.
Hata hivyo, Kenya ilishindwa kutayarisha miundombinu ya mashindano hayo na ikapokonywa huku Morocco ikipewa maandalizi na hatimaye wakatwaa kombe.
Pia mwaka 1996, Kenya kwa mara ya kwanza ilipokezwa maandalizi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), lakini ikapokonywa tena na badala yake ikaelekezwa Afrika Kusini, ambao pia walinyakua ubingwa.
Mashindano ya CHAN ya mwaka huu yanaweka historia kuwa mara ya kwanza kwa Kenya kuandaa fainali za soka barani Afrika.
Kenya itaandaa fainali hizo kwa pamoja na Tanzania na Uganda.
Fursa nyingi zinazoambatana na maandalizi ya mashindano ya CHAN ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu, fursa za kitalii na biashara, na kutangaza Kenya kama kituo bora cha kitalii.
Kuelekea fainali hizi, Kenya imekarabati viwanja vya Nyayo na Kasarani ambavyo kwa pamoja vitatumika kuandaa jumla ya mechi 13 za kindumbwendumbwe cha mwaka huu.
Tanzania itaandaa mechi ya ufunguzi Jumamosi hii kuanzia saa mbili usiku kati ya Taifa Stars na Burkina Faso, katika uwanja wa Benjamin Mkapa, mechi ya kundi B.
Baadaye, siku ya Jumapili, Harambee Stars watapimana nguvu na DR Congo katika uga wa Kasarani kuanzia saa tisa alasiri katika kundi A.
Mashindano mengine makubwa kuwahi kuandaliwa Kenya ni michezo ya Afrika mwaka 1987.