Kenya na Ujerumani zimekubaliana kuongeza ushirikiano wao katika uwekezaji wa nishati safi.
Hatua hiyo inafuatia matokeo ya Mkutano wa Kilele wa Tabi Nchi barani Afrika jijini Nairobi ambapo Ujerumani ilikuwa mmoja wa washirika wakuu.
Nchi hizo mbili zilikubaliana kwamba kuwekeza barani Afrika ni jambo lisiloepukika kutokana na ushindani wake wa hatua za tabia nchi, maendeleo na ukakamavu wa tabia nchi.
Katika mkutano wa pande mbili mjini Berlin kati ya Rais William Ruto na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, amani na usalama katika Upembe wa Afrika ni mambo ambayo pia yalipewa kipaumbele.
Scholz alithamini jukumu muhimu ambalo Kenya inaendelea kutekeleza katika eneo hilo, hasa katika nchi za Sudan, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Somalia.
Kiongozi huyo wa Ujerumani aliutambua mchango wa Kenya katika kujenga uwezo na usaidizi katika chaguzi zijazo nchini DRC na Sudan Kusini.
Rais Ruto alimweleza Kansela Scholz kuhusu juhudi za IGAD kuchukua uongozi katika Mchakato wa Jeddah ambao unaongozwa na Saudi Arabia na Marekani.
Viongozi hao wawili pia walijadili jukumu la Kenya katika kuleta utulivu katika nchi ya Haiti kama sehemu ya Ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama.
Serikali ya Ujerumani ilijitolea kuiunga mkono Kenya katika misheni hiyo.
Rais Ruto na Kansela Scholz walifurahia mijadala inayoendelea kuhusu uhamishaji wa wafanyikazi, jambo linalotazamiwa kukamilika mwaka ujao.
Viongozi hao wawili walikubali kwamba utaratibu wa uhamiaji wenye mpangilio, kama ule unaoendelea kupangwa kati ya Kenya na Ujerumani, utasaidia kukomesha uhamiaji haramu.
Rais Ruto aliitaka Ujerumani kuunga mkono Mageuzi ya Kimataifa ya Fedha ili kupunguza mzigo wa madeni unaozikabili nchi zinazoendelea.
Kenya na Ujerumani zina maslahi makubwa ya pamoja, hasa katika ulinzi wa mazingira, biashara na uwekezaji.
Viongozi hao wawili walikutana siku ya Jumatatu kando ya mkutano wa “G20 Compact with Africa” nchini Ujerumani.
Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi.