Kenya na UAE zashirikiana katika uwekezaji wa kidijitali

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa habari na uchumi wa dijitali Eliud Owalo (kushoto), na mwenzake wa uwekezaji wa Milki za Kiarabu Mohamed Hassan Alsuwaidi.

Kenya na Umoja wa Milki za Kiarabu (UAE), zimetia saini mkataba wa maelewano kuhusu uwekezaji katika masuala ya kidijitali na teknolojia.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Eliud Owalo na Waziri wa Uwekezaji wa UAE Mohamed Hassan Alsuwaidi, walitia saini mkataba huo jijini Abu Dhabi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Owalo aliyekuwa ameandamana na katibu anayesimamia uchumi wa kidijitali katika wizara hiyo mhandisi John Tanui, alisema ushirikiano huo ni hatua kubwa huku pande hizo mbili zikijitolea kufanikisha ushirikiano wa karibu katika uwekezaji na uimarishaji wa miradi ya kidijitali ya miundombinu.

“Uchumi wa kidijitali wa Kenya umeimarika, hatua iliyochochewa na sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia, ICT. Ushirikiano huu utatoa fursa ya uwekezaji wa ICT katika miundombinu ya data na hivyo kutoa nafasi za ajira, pamoja na kuwainua Wakenya walio na ujuzi wa kidijitali,” alisema Owalo.

Kwa upande wake, Alsuwaidi alielezea fursa zilizopo kutokana na ushirikiano wa nchi hizo mbili.

“Kupitia uwekezaji uliolengwa katika miundombinu ya kidijitali, mkataba huu wa maelewano utaharakisha maendeleo katika sekta hii ambayo ina uwezo wa kufanikisha ukuaji katika viwanda,” alisema Alsuwaidi.

Serikali inalenga kuwapa vijana ujuzi wa kidijitali kwa ajili ya ajira zinazohusisha mambo ya kidijitali na ujasiriamali wa kidijitali.

Share This Article