Kenya na Poland kuboresha ushirikiano

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais William Ruto amesema Kenya na Poland zimedhamiria kuboresha ushirikiano katika nyanja mbalimbali zenye maslahi ya pande mbili. 
Amesema mataifa hayo mawili yanakusudia kuboresha ushirikiano katika masuala ya biashara na kiuchumi, kilimo na usalama wa chakula, mazingira na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Poland ni mshirika wa thamani wa Kenya mwenye maadili na matamanio sawa yanayoongoza uhusiano wa sasa na wa siku zijazo,” alisema Rais Ruto.
Aliyasema hayo wakati akiwahutubia wanahabari akiwa pamoja na Rais Andrzej Duda wa Poland, ambaye yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili.
Kwa upande wake, Rais Duda alisema Poland inadhamiria kukuza uhusiano thabiti kati yake na Kenya.
“Hii si ziara ya heshima, hii ni ziara ambayo inaleta uwezo mkubwa wa kiuchumi unaoweza kufanyika kwa ajili ya siku zijazo,” alisema Rais Duda.
Viongozi hao wawili walishuhudia kutiwa saini kwa Mkataba wa Maelewano juu ya umoja wa kodi, kilimo na maendeleo ya vijiji.
Rais Ruto and Rais Duda walikubaliana kuongeza ushirikiano katika sekta za kilimo na usalama wa chakula ili kupunguza pengo la mahitaji ya ngano na bidhaa za nafaka nchini Kenya.
Share This Article